Muasisi
na Mwenyekiti wa kwanza wa Chama cha Wananchi (CUF), James Mapalala,
amesema yanayotokea ndani ya chama hicho hayamshangazi kwa kuwa Katibu
Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad alitumia watu ‘walevi’ kumfukuza ndani ya
chama hicho mwaka 1994.
Akizungumza kwa njia ya simu na Tanzania
Daima, Mapalala alisema Maalim Seif ni kiongozi anayewatumia baadhi ya
wanachama wake kupata mafanikio, na kisha hutumia nguvu kuwafukuzwa kwa
vitimbi kama alivyofanyiwa yeye na sasa Hamad Rashid Mohamed.
Alidai
kuwa Maalim Seif aliwahi kumtumia yeye kama daraja mwaka 1992 kwa
kuzunguka nchi nzima bara na Zanzibar, akilala vijijini kwa lengo la
kukitangaza chama ili waweze kuwakomboa wananchi wanyonge lakini matokeo
yake alimfukuza kwa visingizio mbalimbali ambavyo si vya kweli.
Mapalala
alienda mbali zaidi na kueleza kuwa Maalim Seif si mtu wa kawaida hasa
unapogusia masuala ya madaraka kwa kuwa ni mtu ambaye anapenda fedha na
madaraka, huku akiyatumia vibaya kwa kuwakandamiza wanyonge, “Hakuna mtu
ndani ya CUF asiyejua kwamba Hamad Rashid alikuwa ni mtu muhimu sana
ndani ya chama hicho kwani ndiye kiongozi wa pekee mwenye uwezo wa
kutafuta fedha nje ya nchi kwa ajili ya kuendesha chama, lakini Maalim
amemtimua kama ilivyokuwa kwangu baada ya kufanikiwa kupata mafanikio
mbalimbali hadi kuwa Makamu wa Rais,” alisema Mapalala.
Mapalala
alidai kuwa Maalim Seif anapenda kila atakalosema yeye ndilo litendwe na
watu wote ndani ya chama bila kuzingatia maoni ya watu wengine hata
kama si jambo zuri kwa maslahi ya chama.
Akizungumzia kufukuzwa
kwake ndani ya chama, alisema kuwa mwaka 1994 katika mkutano
uliyofanyika mkoani Tanga alitimuliwa bila kupewa sababu za msingi na
kwamba waliofanya maamuzi katika mkutano huo hawakuwa wanachama halali
na nakala za barua na majina yao anayo hadi sasa.
Aidha aliwaonya
viongozi mbalimbali wa CUF kuwa wanapozungumzia matatizo yao ndani ya
chama hasa katika kipindi hiki ambacho wamemfukuza Hamad wasitolee mfano
jina lake kwa kuwa ana vielelezo vyote vya Maalim Seif na wenzake
kutumia ‘walevi’ wa pombe ambao walihongwa huku wakiwa si wajumbe ili
waweze kunifukuza, “Tena sitaki kabisa wasijipe umaarufu kusafisha
dhambi zao kwa kunitaja mimi. Katika mkutano ule wa Tanga waliokuwa
wameitisha kwa ajili ya kunifukuza mimi, nilipewa barua masaa machache
na kwamba mkutano ulifanyika usiku, wajumbe walikuwa si halali na
vielelezo hadi sasa ninavyo wasitake niwaumbue,” alisema Mapalala.
Mapalala
alisema Maalim Seif bila kujiingiza katika migogoro alitakiwa kuangalia
hali ya wananchi wa Zanzibar hasa Pemba ambao tangu kuingia kwa
serikali ya mseto mambo ndiyo yamezidi kuwa magumu zaidi, “Sharif Hamad
ni kiongozi ndani ya CCM ndio maana anashindwa kuwatetea wananchi, ameua
chama; watu wanahoji anakuja juu, watu wanahoji matumizi ya fedha
anakuja juu, ni mtu ambaye anapenda sana madaraka na hili ndilo tatizo
kubwa ambalo linaua demokrasia ndani ya vyama hasahasa chama hicho,”
alisema Mapalala.
Aidha alimshauri mbunge huyo wa Wawi kama ana
nia ya kuwakomboa wananchi hasa wakazi wa Pemba basi aendelee kwa
kuanzisha chama chake asirudi CCM kwa kuwa chama hicho ndicho kimeungana
na Maalim Seif.
Mapalala ambaye ni mwenyekiti wa chama cha
Chausta amemkaribisha Hamad Rashid kujiunga nacho kwa vile anaamini ni
kiongozi makini na mchapa kazi hodari.
---
via
Tanzania Daima