FIND UR TRUE LOVE

Saturday, January 7, 2012


 
 
 
Muasisi na Mwenyekiti wa kwanza wa Chama cha Wananchi (CUF), James Mapalala, amesema yanayotokea ndani ya chama hicho hayamshangazi kwa kuwa Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad alitumia watu ‘walevi’ kumfukuza ndani ya chama hicho mwaka 1994.

Akizungumza kwa njia ya simu na Tanzania Daima, Mapalala alisema Maalim Seif ni kiongozi anayewatumia baadhi ya wanachama wake kupata mafanikio, na kisha hutumia nguvu kuwafukuzwa kwa vitimbi kama alivyofanyiwa yeye na sasa Hamad Rashid Mohamed.

Alidai kuwa Maalim Seif aliwahi kumtumia yeye kama daraja mwaka 1992 kwa kuzunguka nchi nzima bara na Zanzibar, akilala vijijini kwa lengo la kukitangaza chama ili waweze kuwakomboa wananchi wanyonge lakini matokeo yake alimfukuza kwa visingizio mbalimbali ambavyo si vya kweli.

Mapalala alienda mbali zaidi na kueleza kuwa Maalim Seif si mtu wa kawaida hasa unapogusia masuala ya madaraka kwa kuwa ni mtu ambaye anapenda fedha na madaraka, huku akiyatumia vibaya kwa kuwakandamiza wanyonge, “Hakuna mtu ndani ya CUF asiyejua kwamba Hamad Rashid alikuwa ni mtu muhimu sana ndani ya chama hicho kwani ndiye kiongozi wa pekee mwenye uwezo wa kutafuta fedha nje ya nchi kwa ajili ya kuendesha chama, lakini Maalim amemtimua kama ilivyokuwa kwangu baada ya kufanikiwa kupata mafanikio mbalimbali hadi kuwa Makamu wa Rais,” alisema Mapalala.

Mapalala alidai kuwa Maalim Seif anapenda kila atakalosema yeye ndilo litendwe na watu wote ndani ya chama bila kuzingatia maoni ya watu wengine hata kama si jambo zuri kwa maslahi ya chama.

Akizungumzia kufukuzwa kwake ndani ya chama, alisema kuwa mwaka 1994 katika mkutano uliyofanyika mkoani Tanga alitimuliwa bila kupewa sababu za msingi na kwamba waliofanya maamuzi katika mkutano huo hawakuwa wanachama halali na nakala za barua na majina yao anayo hadi sasa.

Aidha aliwaonya viongozi mbalimbali wa CUF kuwa wanapozungumzia matatizo yao ndani ya chama hasa katika kipindi hiki ambacho wamemfukuza Hamad wasitolee mfano jina lake kwa kuwa ana vielelezo vyote vya Maalim Seif na wenzake kutumia ‘walevi’ wa pombe ambao walihongwa huku wakiwa si wajumbe ili waweze kunifukuza, “Tena sitaki kabisa wasijipe umaarufu kusafisha dhambi zao kwa kunitaja mimi. Katika mkutano ule wa Tanga waliokuwa wameitisha kwa ajili ya kunifukuza mimi, nilipewa barua masaa machache na kwamba mkutano ulifanyika usiku, wajumbe walikuwa si halali na vielelezo hadi sasa ninavyo wasitake niwaumbue,” alisema Mapalala.

Mapalala alisema Maalim Seif bila kujiingiza katika migogoro alitakiwa kuangalia hali ya wananchi wa Zanzibar hasa Pemba ambao tangu kuingia kwa serikali ya mseto mambo ndiyo yamezidi kuwa magumu zaidi, “Sharif Hamad ni kiongozi ndani ya CCM ndio maana anashindwa kuwatetea wananchi, ameua chama; watu wanahoji anakuja juu, watu wanahoji matumizi ya fedha anakuja juu, ni mtu ambaye anapenda sana madaraka na hili ndilo tatizo kubwa ambalo linaua demokrasia ndani ya vyama hasahasa chama hicho,” alisema Mapalala.

Aidha alimshauri mbunge huyo wa Wawi kama ana nia ya kuwakomboa wananchi hasa wakazi wa Pemba basi aendelee kwa kuanzisha chama chake asirudi CCM kwa kuwa chama hicho ndicho kimeungana na Maalim Seif.

Mapalala ambaye ni mwenyekiti wa chama cha Chausta amemkaribisha Hamad Rashid kujiunga nacho kwa vile anaamini ni kiongozi makini na mchapa kazi hodari.
---
via  Tanzania Daima
 
 
Picture
photo by "Bellringersly" via flickr
Huko Dodoma, madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma wameendelea na msimamo wa kutofanya kazi hadi watakapolipwa fedha zao huku utoaji wa huduma kwa wagonjwa ukiendelea kudorora.

Mgomo huo wa madaktari ambao ulianza juzi asubuhi umesababisha wagonjwa wengi waliolazwa na wale wanaofika hospitalini hapo kukosa huduma zinazostahili.

Madaktari hao wamegoma wakishinikiza Wizara ya Afya iwalipe fedha zao za miezi miwili wanazodai.

Zaidi ya madaktari 33 wanaidai wizara hiyo malipo ya fedha kuanzia mwezi Novemba na Desemba mwaka jana ambazo hawajalipwa hadi leo.

Hata hivyo, kaimu mganga mkuu wa hospitali ya mkoa, Dkt. Nassoro Mzee, alisema malipo ya madaktari hao yanashughulikiwa baada ya fedha kufikishwa Hazina ndogo ya Dodoma, “Fedha zimeshafika na zipo kwenye utaratibu wa malipo, naamini hadi Jumatatu madaktari wote watakuwa wamelipwa fedha zao,” alisema.

Hata hivyo, katibu wa hospitali hiyo, Isaack Kaneno, alisema madaktari hao wamekataa kuingia kazini hadi wapate fedha mkononi, licha ya kuambiwa kuwa ziko Hazina na zinashughulikiwa, “Inasikitisha kwamba wenyewe wanadai mwezi mmoja na hapohapo kuna watumishi wengine wa serikali wanadai miezi mingi, mbona hawajagoma?” alisema.

Hata hivyo, katibu mkuu alisema kwa mujibu wa taratibbu za kazi, mfanyakazi akigoma kwa siku tatu mfululizo atakuwa amejifuta kazi mwenyewe.

- via Tanzania Daima
 
 
Picture
photo by "MADAKTARI" via flickr
Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) umewapa barua za kurudi Wizara ya Afya madaktari 229 walioko katika mafunzo kwa njia ya vitendo kutokana na mgomo wa siku nne wakishinikiza kulipwa posho zao za mwezi mmoja.

Hatua ya kuwafukuza madaktari hao kwa barua hizo, imesababisha huduma za afya kudorora na kuna madai kwamba baadhi ya wagonjwa walikosa huduma kwa siku nzima ya jana kutokana na kutokuwepo kwa madaktari.

Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dkt. Marina Njelekela, tangu juzi alikataa kuzungumza na waandishi wa habari, na kutwa nzima ya jana simu yake ya kiganjani ilikuwa ikiita bila kupokelewa.

Madaktari hao walifukuzwa kupitia tangazo la barua iliyosainiwa na Dkt. Marina Njelekela kisha kubandikwa katika kila wodi za hospitali hiyo likibeba kichwa cha habari: ‘Kuhusu kurudishwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii’.

Kwa mujibu wa tangazo, uongozi wa Muhimbili umewataka madaktari hao kuchukua barua zao ili waende Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupangiwa kazi katika vituo vingine, kwa vile hawatakiwi tena pia.

“Mara upatapo barua hii unatakiwa kujeresha vifaa vyote ulivyopewa na hospitali vikiwemo funguo za chumba na kitambulisho na kuripoti Wizara ya afya mara moja,” ilisema sehemu ya barua hiyo ambayo nakala yake pia imepelekwa kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi Jamii, Blandina Nyoni.

Kwa mujibu wa barua hiyo madaktari hao wamekiuka makubaliano ya kifungu namba 1(b)(d) (e) (f) (g) kama ilivyoelekezwa na Katibu Mkuu katika barua yake ya kuwapangia mafunzo katika Hospitali ya Muhimbili.

Habari kutoka ndani ya hospitali hiyo zinaeleza kwamba madaktari hao walirejea kazini jana majira ya saa 11.00 alfajiri wakiwa wamevalia nguo zao za kazi na kabla hawajaingia wodini walizuiwa na walinzi wakitakiwa kuangalia matangazo yaliyoeleza kusimamishwa kwao kazi.

Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo kiongozi wa madaktari hao wanafunzi, Dkt. Deogratias Mally, alisema wanashangazwa na hatua ya uongozi kuwasimamisha kazi wakati mkataba wao unatambuliwa na Wizara ya Afya.

Alisema wakati wanadai haki yao hawakuitisha mgomo, hivyo wanashangazwa na hatua ya uongozi huo kuingilia suala ambalo lilitakiwa kufanywa na wizara kwani hata mkataba wao wa ajira hausemi hivyo, “Barua ya madai yetu tuliandika kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na si Mkurugenzi wa Muhimbili,” alisema Dk. Mally.

Alisema kutokana na hali hiyo jana walijipanga kumtafuta mwanasheria na kukaa naye ili watafakari walipokosea ili baada ya kikao na mwanasheria huyo Jumatatu ijayo waende wizarani.

Mgomo huo wa madaktari ulianza mwanzoni mwa wiki hii kwa madaktari hao kushinikiza kulipwa jumla ya sh milioni 176 ambazo ni posho zao za kujikimu za mwezi Desemba mwaka jana. Kwa maelezo yao walidai hawatamaliza mgomo huo hadi hapo watakapolipwa fedha hizo. Hata hivyo juzi jioni walianza kulipwa baada ya serikali kusalimu amri.


via Tanzania Daima

No comments: